Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

State Mining Corporation

State Mining Corporation

News

STAMICO YAINGIA MAKUBALIANO NA KAMPUNI YA SUNESS KUENDELEZA MRADI WA SHABA


Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limesaini Makubaliano ya awali na Kampuni ya Suness Limited ya nchini Italia kwa ajili ya kuendeleza mradi mkubwa wa shaba (copper) katika Mkoa Kilimanjaro.

Utiaji saini wa makubaliano hayo umefanyika Mapema Desemba 2021 wakati wa mkutano wa Wafanyabiashara na Wawekezaji Watanzania na Italia kwenye jukwaa la Biashara na uwekezaji nchini Italia na kushuhudiwa na Naibu Waziri wa Madini Mhe. Prof.Shukrani Manya.

Akiongea mara baada ya utiaji saini Prof. Manya ameipongeza STAMICO kwa hatua hii ya kufungua milango kwa wawekezaji katika sekta ya madini nchini.

Kwa upande wa STAMICO,

Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse amesema makubaliano haya ni mwanzo mzuri kwa Shirika na ni muendelezo wa kuongeza thamani katika mnyororo wa sekta ya madini kwa kuwa STAMICO ina vitalu vya Shaba vyenye leseni vinavyohitaji kuendelezwa.

Dkt. Mwasse ametumia fursa hiyo kuelezea kwa kina juu ya mradi mkubwa wa madini ya shaba yanayopatikana katika Mkoa wa Kilimanjaro ambapo umewavutia wawekezaji hao ambao wameonesha nia ya kuingia ubia na Shirika.

“Shirika lina mradi wake mkubwa wa madini wenye kiasi kikubwa cha mashapu ya Shaba na kupitia Jukwa hili tumeweza kuwavuta wawekezaji hadi kufikia hatua ya kusaini makubaliano ya awali kabla ya kuzuru Tanzania kwa ajili ya kukamilisha makubaliano haya. Amesema Dkt. Mwasse

Aidha, Rais wa Kampuni ya Sunless Bw. Sandro Calo amesema kampuni yake imejikita katika sekta ya madini na kwamba amefurahishwa na hatua hii ya utiaji saini wa awali wa makubaliano hayo yatakayowezesha kushirikiana na Serikali ya Tanzania.

Utiaji saini wa makubaliano haya yameshuhudiwa na Naibu Waziri, Wizara ya Madini Mhe. Prof. Shukrani Manya, Balozi wa Tanzania Nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabiti Kombo, Mkurugenzi Idara ya Diplomasia ya Uchumi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Edwin Rutageruka pamoja na Mkurugenzi wa Kampuni ya Utalii ya Zanzibar Classic Safaris, Bw. Yussuf Salim Njama.