Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

State Mining Corporation

State Mining Corporation

News

STAMICO yatoa Mafunzo kwa Wachimbaji Wadogo wenye Usikivu Hafifu


Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limetoa tena mafunzo ya Uchimbaji, Usalama Migodini na Biashara ya Madini kwa wachimbaji wadogo wenye usikivu hafifu (viziwi) katika mkoa wa Mbeya mapema mwezi Novemba 2021


Akiongea wakati wa kufunga mafunzo haya Mkuu wa Wilaya ya Mbeya bw. Rashid Chuachua ameipongeza STAMICO kwa kutoa mafunzo hayo kwa wachimbaji wa kundi hilo mbalo ni nguvu kazi muhimu kwa Taifa kwa kuwa mara nyingi wamekuwa wakishaulika.


Amefurahia jinsi STAMICO ilivyoamua kuwakumbuka wachimbaji wenye usikivu hafifu kwa kuwapa mafunzo haya adhimu yatakayowasaidia kubadilisha mfumo wao wa uchimbaji na kuachana na uchimbaji duni usio na tija.


Ametoa wito kwa washiriki wa mafunzo haya kutumia elimu waliyoipata katika kazi zao huku wakizingatia utunzaji wa mazingira kwa kuwa wengi wao wametoka katika maeneo yenye madini.


Kwa upande wa STAMICO Meneja wa Uchimbaji Mdogo bw. Tuna Bandoma amesema mafunzo haya yametolewa ili kuwajengea uwezo wachimbaji wenye usikivu hafifu ili waweze kufanya kazi cha uchimbaji wenye tija sawa na watu wengine.


Bandoma amesema mafunzo haya ni muendelezo wa mafunzo yanayotolewa kwa wachimbaji wadogo ambayo yamo katika mkakati wa Shirika wa kuwaendeleza wachimbaji wadogo nchini na yameleta muitikio chanya kwa maeneo ambayo yameshafanyika hivyo yataendelea kufanyika katika maeneo mengine nchini.


Amesema wachimbaji hawa wamepatiwa mafunzo ikiwa ni hatua ya awali katika kuwasaidia, STAMICO itaendelea nao ili kuhakikisha wanafika hatua nzuri katika suala nzima la uchimbaji.


Akiongea kwa niaba ya wachimbaji bw. Kelvin Nyema Mkurugenzi wa Taasisi ya maendeleo ya Viziwi Tanzania (TAMAVITA) Cha wameishukuru STAMICO kwa kuendelea kuwasaidia wachimbaji wenye usikivu hafifu katika mambo mbalimbali yanayohusu uchimbaji yakiwemo mafunzo, vifaa ya kiusalama na kuwawezesha kupata maeneo yatakayowawezesha kujikwamu kutoka katika hali duni ya kiuchimbaji.


“STAMICO imekuwa nasi bega kwa bega, tunaishukuru sana kwa kuendelea kutusaidia kuanzia mwanzo hadi sasa tulipofikia, kwa kutupa elimu ya utambuzi wa miamba ya dhahabu, uchimbaji salama na biashara ya madini katika maeneo mbalimbali” alisisitiza Nyema


Amesema mafunzo haya yatawasaidia sana wachimbaji wadogo katika shughuli zao za kila siku na kuahidi kuwa wachimbaji hawa wataenda kuwa mabalozi wazuri kwa wachimbaji wengine ambao hakupata nafasi ya kushiriki katika mafunzo haya.


Wachimbaji hao wametoa ombi kwa STAMICO kuendelea kuwasaidia kupata maeneo ya uchimbaji ili waweze kuondokana na unyanyasaji wanaoupata wakiwa wanafanya kazi chini ya watu wengine kutokana na hali yao ya kutosikia.


STAMICO imetoa mafunzo kwa wachimbaji wapatao 48 kutoka mikoa ya Mbeya na Songwe. Mafunzo haya ni awamu ya Pili ambapo awamu ya kwanza yalifanyika mkoani Geita yakiwa na lengo la kuwashirikisha kikamilifu watu wenye usikivu hafifu katika shughuli za uchimbaji wenye tija.