News
STAMICO YATWAA TUZO YA KUJALI JAMII
Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limetwaa Tuzo ya Kujali Jamii (CSR for Women Empowerment) katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 28 Februari,2025.
Tuzo hiyo iliyokabidhiwa na Mgeni Rasmi, Mhe. Doto Mashaka Biteko, Naibu Waziri Nkuu na Waziri wa Nishati, imeitambua STAMICO kama kinara wa kuwezesha wanawake katika sekta ya madini nchini.
Tuzo hiyo ilipokelewa na Mkurugenzi wa STAMICO wa Rasilimali Watu,Bw Deusdedith Magalla kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji,Dkt Venance Mwasse.
STAMICO ilitajwa kuwezesha wanawake kwa kuwapa uwakala wa nishati ya kupikia ya Rafiki Briquettes vikundi 16 vya Wanawake na Samia.
Pia Shirika limevipatia vikundi sita kontena za futi 40 ili kurahisisha kusambaza nishati hii nchini kote.
Vikundi hivyo ni kutoka mikoa ya Geita,Dodoma,Mbeya,Iringa,Songwe,Ruvuma na Njombe.
Shirika pia limeipatia taasisi ya Foundation for Disabilities Hope (FDH) iliyopo Dodoma inayohudumia watu wenye ualbino kontena la futi 40 pamoja na uwakala wa kusambaza nishati hiyo.
Katika azma yake ya kujali mazingira,STAMICO imeshirikiana na vikundi vya Wanawake na Samia maeneo mbalimbali Tanzania Bara na Visiwani kupanda miti.
Tuzo hiyo ni sehemu ya maandalizi ya Siku ya Kimataifa Duniani (PreIWD) inayoadhimishwa tarehe 8 Machi.
Tanzania itaadhimisha siku hii kitaifa jijini Arusha.