Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Madini la Taifa

FEMATA YASHAURIWA KUFANYA UTAFITI WA MASOKO YA MADINI NCHINI

Imewekwa: 27 April, 2026
FEMATA YASHAURIWA KUFANYA UTAFITI WA MASOKO YA MADINI NCHINI

Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania ( FEMATA ) limeshauriwa kuanza kufanya utafiti wa masoko ya madini ndani na nje ya nchi ili kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata tija zaidi kutokana na rasilimali madini zilizopo nchini.

Ushauri huo umetolewa na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde katika Mkutano maalum uliofanyika jijini Dodoma tarehe 24 Aprili, 2026 uliohusisha Shirikisho la FEMATA na wataalamu wa Wizara ya Madini ukiwa na lengo la kujadili mkakati wa Uchumi wa kufikia dola trilioni moja.

Waziri Mavunde ameongeza kuwa, kuwepo kwa utafiti huo kutasaidia wachimbaji wadogo kufahamu mnyororo wa thamani na bei elekezi za kitaifa, jambo litakalo punguza utegemezi kwa madalali wanaonunua madini kwa bei ya nchi.

Waziri Mavunde amefafanua kuwa, kwasasa Serikali inakuja na mpango kamili utakaoanzia utafiti wa awali utakaofanywa na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti  wa Madini Tanzania ( GST ) ambao utaendeleza utafiti wa kina kwa lengo la kuvumbua maeneo mapya ya rasilimali madini.

Aidha, Waziri Mavunde ameitaka FEMATA kuongeza mashirikiano na Taasisi za Wizara ya Madini katika kukusanya takwimu ili kuongeza ufahamu kwa Wanachama wake hususani katika taarifa za mwenendo wa sekta ya Madini kwenye utafiti, uchimbaji, uchenjuaji na masoko.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini  Dkt. Steven Kiruswa, amemuelekeza Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini kuandaa utaratibu mzuri wa kugawa leseni zilizofutwa kwa wachimbaji wadogo kwenye maeneo yao ili kuongeza tija ya uzalishaji madini kila mkoa.

Naye Mkuregenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse, ameishauri FEMATA kuendelea na mpango wake wa kufungua Benki ya Madini ili kupunguza changamoto za kiuchumi zinazowakabili wachimbaji wadogo katika shughuli zao.

Akizungumza kwa niaba ya wachimbaji wadogo nchini, Rais wa FEMATA Bw. John Bina ameishukuru Wizara ya Madini kwa ushauri na ushirikiano mzuri inayotoa kwa wachimbaji wadogo kuanzia vifaa, mashine za uchorongaji miamba na kuwaunganisha na Taasisi za kifedha jambo linaloleta mageuzi makubwa kwa wachimbaji nchini.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo