News
GGML YAIPIGA MSASA STAMICO USALAMA MAHALA PA KAZI, MGODINI
●Yatoa mafunzo kuhusu mazingira hatarishi kwa usalama wa wafanyakazi
● Yahimiza kufanya kazi kwa kuzingatia na kuacha mazoea kazini
Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) leo oktoba 9, 2024 limepata mafunzo ya usalama mahala pa kazi, hususani sehemu za migodini ili kuweza kujikinga na athari mbalimbali zinazoweza kutokea kwa mtu binafsi na wategemezi
Mafunzo haya yametolewa na wataalamu kutoka kampuni ya Uchimbaji Madini ya Geita Gold Mine Limited (GGML) yakilenga kuwakumbusha wafanyakazi wa STAMICO umuhimu wa kuzingatia matumizi ya alama za kimazingira na vifaa kinga mahala pa kazi hususani migodini.
Akiongea kuhusu mafunzo hayo Bw. Deusdedith Magala ameishukuru Kampuni ya GGML kwa kuamua kuwafikia na kuwapa elimu ya usalama kwa watumishi wote wa STAMICO ili kuwajengea uelewa wa kujikinga na ajali.
Amesema mafunzo hayo yamehimiza ufanyaji kazi unaozingatia mipaka ya utendaji kazi, kuacha kufanya kazi kwa mazoea na kudhania ili kuepusha ajali.
Naye, Bi. Ashura Said Mratibu wa Mafunzo hayo amesema ni muhimu kwa Shirika kuzingatia usalama mahala pa kazi ili kuwalinda wafanyakazi wake na athari zinazoweza kuwapata.
Amesema ni lazima kuhakikisha kuwepo kwa mazingira ya kazi ambayo ni salama kwa mfanyakazi kufanya kazi ili kuweza kufikia malengo kwa kuzingatia sera ya usalama mahala pa kazi
Amesisitiza kuwepo kwa mikakati ya kukabiliana na dharura pindi inapotokea ili kuepusha athari kubwa zaidi
Amehimiza kuwepo kwa Mawasiliano kuhusu jambo au mabadiliko yoyote ya kimazingira yanayofanyika ili kila mtu aweze kuyatambua na kuyafanyia kazi.
Kwa upande wa wafanyakazi Mohamed Kaunya ameushùkuru uongozi wa STAMICO kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo yamelenga kuwakumbusha wajibu wa kila mfanyakazi katika kuzingatia usalama mahali pa kazi.
Mafunzo haya ya siku mbili ya Usalama na Afya mahali pa kazi kwa wafanyakazi wote wa STAMICO yameandaliwa kwa kushirikiana na Geita Gold Mine kwa kuanzia wafanyakazi waliopo Dar es salaam na baadae itafanyika kwa wafanyakazi wake wote wa
Kiwira, Itumbi ( Chunya), Dodoma, Shanta, Lwamgasa, Buckreef na Katente.