KIWANDA CHA KUCHAKATA MADINI CHUMVI MBIONI KUKAMILIKA MKOANI LINDI
Katika juhudi za kuendeleza na kuboresha uzalishaji wa madini chumvi , Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa ( STAMICO ) ipo mbioni kukamilisha kiwanda cha kuchakata madini chumvi katika Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi pamoja na kusaidia ujenzi wa viwanda katika Mikoa ya Tanga na Mtwara.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde wakati wa kikao baina ya Chama cha Wazalishaji Chumvi Tanzania ( TASPA ) na Wizara ya Madini na Taasisi zake kilichofanyika jijini Dodoma Aprili 23, 2026.
Waziri Mavunde amesema kuwa, Serikali ilipokea maombi ya TASPA na kufanikiwa kushusha mrabaha katika madini chumvi kutoka asilimia 4 mpaka asilimia 1 ya bei elekezi.
Waziri Mavunde ameongeza kuwa, Serikali inaendelea kushughulikia uanzishwaji wa leseni moja katika shamba moja, lengo ni kutofautisha na madini mengine ikiwa pamoja na kuongeza uzalishaji wa chumvi bora nchini.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa ( STAMICO ) Dkt. Venance Mwasse amesema kuwa, miundombinu ndani ya kiwanda imekamilika kwa asilimia kubwa.
Dkt. Mwasse ameongeza kuwa, kiwanda kitakuwa na uwezo wa kupokea chumvi ghafi kutoka kwa wazalishaji kuanzia 50 hadi 60 kwa siku.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TASPA Bi. Hawa Ghasia ameishukuru Serikali kwa kuwezesha mazingira bora ya uvunaji wa chumvi ikiwa pamoja na kupanda kwa bei ya chumvi baada ya kuwepo kwa zuio la uingizwaji wa chumvi ghafi kiholela kutoka nje ya nchi.
Kiwanda cha kuchakata chumvi Mkoani Lindi pindi kitakapoanza kazi kinatarajia kuchakata tani 60 hadi 100 kwa siku.