STAMICO NA RANGERS EXPLORATION ZAINGIA MKATABA WA KUTAFITI MADINI YA SHABA
Katika hatua kubwa ya kimkakati, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limechukua hatua nyingine muhimu kuelekea uchimbaji mkubwa nchini kwa kusaini mkataba wa miaka minne na kampuni ya Rangers Exploration kutoka Mauritius kwa ajili ya kufanya utafiti wa madini ya shaba katika leseni yake ya Changube, Mkoani Kilimanjaro.
Hafla hiyo ya kihistoria imefanyika Mei 20, 2026, jijini Dar es Salaam. Na kushuhudiwa na Kamishna Msaidizi wa Madini, Bw. Terrence Ngole, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Bw. Ngole alibainisha kuwa mwelekeo wa Tanzania kwa sasa ni kuwekeza kwenye madini ya kimkakati kama shaba. Madini haya hivi sasa yana soko kubwa na thamani kubwa duniani. Mkataba huu unafungua milango ya kuelekea kwenye uchimbaji Mkubwa.
Aidha, Bw Ngole aliipongeza STAMICO kwa kusimamia vizuri miradi katika sekta ya madini na akaupongeza Ubia huu kuwa ni Ubia mzuri na wa kimkakati katika mashirikiano yote ambayo STAMICO imeingia hivi karibuni.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse, alieleza kuwa mkataba huu ni mwendelezo wa azma ya Shirika hilo kujikita kwenye uchimbaji mkubwa hususani kwenye madini ya kimkakati. STAMICO imedhamiria kutumia leseni zake vizuri ili kuvutia wawekezaji wenye tija kwa maendeleo ya nchi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa STAMICO, Balozi IGP Mstaafu Simon Nyakoro Sirro, amewakaribisha wawekezaji hao na kuahidi kuwapa ushirikiano wawekezaji hawa na pia ameupongeza uongozi wa STAMICO kwa kuendelea kusimamia rasilimali za Shirika vizuri
Balizi Sirro amesisitiza kuwa shughuli za utafiti ni vizuri zianze mara moja ili taifa lianze kufaidika na rasilimali hizo mapema.
Kwa upande wa wekezaji hao, Mkurugenzi Mtendaji wa Rangers Exploration, Bw. Allan Mulligan, alieleza furaha yake kufikia makubaliano hayo. Ameahidi kuwa kampuni yake itatumia fursa hiyo kuboresha eneo la mradi na kuendelea kuwekeza zaidi kwenye sekta ya madini nchini Tanzania.
Hatua hii inaashiria ufanisi mkubwa wa STAMICO katika kuvutia uwekezaji mkubwa wenye tija kwa taifa.