STAMICO YAENDELEA KUFANYA MAGEUZI KWA WANAWAKE SEKTA YA MADINI
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde amelipongeza Shirika la Madini la Taifa ( STAMICO ) kwa kuwalea na kuwaendeleza kwa vitendo wachimbaji wa madini Wanawake nchini.
Pongezi hizo amezitoa katika hafla iliyofanyika tarehe 23 Aprili, 2026 jijini Dodoma ya kukabidhi pampu 10 za kisasa za kutolea maji mgodini kwa wachimbaji wadogo Wanawake kwa ajili ya kurahisisha shughuli za uchimbaji madini.
Amesema kuwa, Serikali itaendelea kuwapatia akina Mama leseni na katika leseni 40 zilizofutwa, Wanawake watapewa kipaumbele hasa wa TAWOMA.
Mhe. Mavunde ameitaka STAMICO kuongeza mashine za kusaga mawe ( Jaw Crushers ) kwa akina Mama ili wasiendelee kutumia teknolojia duni zikiwemo nyundo.
Ameongeza kuwa, STAMICO iwanunulie mashine za kupata takwimu za kijiofizikia ( Drones ) zitakazowasaidia wachimbaji wadogo kuwa na takwimu sahihi za maeneo yao.
Akizungumza kwa upande wa STAMICO, Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Venance Mwasse ameahidi kuendelea kuwapa ushirikiano na kuunga mkono jitihada za kuwainua Wanawake kwenye sekta ya Madini.
Dkt. Mwasse alisema kuwa, waliomba pampu 17 na leo pampu 10 zimekabidhiwa na Mwezi wa tano, Waziri atakabidhi pampu saba zilizobakia.
Ametoa rai kwa wadau wengine kama vile CRDB, AZANIA, GF TRUCKS, PACT na wengine kujitokeza kuwashika mkono Wanawake wachimbaji.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wanawake ( TAWOMA ) Bi. Semeni John Malale ameishukuru na kuipongeza STAMICO kwa kuwa mlezi wao wa karibu sana.
STAMICO inaendelea kutekeleza jukumu lake la ulezi wa Wachimbaji wadogo ikiweka nguvu katika kuhakikisha makundi maalum ya Wanawake, Vijana na watu wenye mahitaji maalum yanapewa kipaumbele katika ushiriki wao katika mnyororo mzima wa madini.