STAMICO YATEKELEZA AHADI ZA MHESHIMIWA RAIS SAMIA KWA KISHINDO TABORA
Shirika la Madini la Taifa ( STAMICO ) limezindua Kiwanda chake cha Nishati safi ya Rafiki Briquettes kilichopo katika eneo la Kiloleni Mkoani Tabora na pia kutoa uwakala na kugawa Kontena za kuhifadhia na kuuzia Nishati hiyo kwa Vikundi vya Wanawake na Samia katika Mikoa mitano ya Tabora, Kigoma, Rukwa, Katavi na Singida.
Akiongea kabla ya uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse alimueleza Mgeni Rasmi na wageni waalikwa kuhusiana na jinsi STAMICO inavyoendelea kujipambanua kama kinara wa kuongoza kampeni ya matumizi ya Nishati safi.
Dkt. Mwasse alieleza jinsi STAMICO ilivyoanza kwa kufanya utafiti wa kutumia vumbi la Makaa ya Mawe ambalo hupitishwa kwenye mchakato wa Kiwandani kupunguza gesi zisizofaa kwa matumizi ya binadamu na kutengeneza Nishati safi ya Rafiki Briquettes ambayo hutumiwa majumbani na pia kukausha mazao.
Dkt. Mwasse aliongelea utafiti uliofanyika katika kukaushia Tumbaku na matokeo mazuri ambayo yameonyesha ufanisi mkubwa wa Nishati ya Rafiki Briquettes. Aliongeza kwa kusema kuwa, Kiwanda hiki chenye uwezo wa kuzalisha tani 20 kwa saa, kimejengwa mahsusi kuhakikisha kinaleta suliuhisho katika matumizi ya Nishati safi kwa wakulima wa Tumbaku. Aliongeza kwa kusema kuwa, wakulima wa Tumbaku wamekuwa wakitumia kuni kukaushia Tumbaku jambo ambalo linaharibu mazingira, hivyo kwa ujio wa Rafiki Briquettes italeta tija ambapo kwa majaribio yaliyofanyika ambayo wakulima wenyewe wameyashudia italeta suluhisho la kudumu kwa wakulima , Taasisi na watu binafsi ambao watafaidika na matumizi ya Nishati safi.
Alimalizia kwa kuahidi kuwapa kipaumbele wazawa wa Tabora katika ajira na fursa za kufanya biashara na Kiwanda hiki cha Rafiki Briquettes. Kwa kuanzia Kiwanda kitaajiri watu 50 na kutakuwa na ajira zaidi ya hizo kwa siku za mbeleni.
Kwa upande wake Mgeni Rasmi Mhe: Anthony Mavunde, Waziri wa Madini, baada ya kuzindua Kiwanda hicho, aliipongeza STAMICO kwa kwa hatua hii ambayo imeendana na utekelezaji wa ahadi za Mhe: Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan alizoahidi kutekeleza ndani ya siku 100 za kwanza za Muhula wake wa pili wa Uongozi.
Mhe: Mavunde ameeleza kuwa, Kiwanda hicho kilichojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 3, kitawanufaisha Wakulima wa Tumbaku wanaozalisha wastani wat ani 95,000 kwa Mwaka ambazo awali walikabiliwa na changamoto ya kukausha Tumbaku kwa kutumia kuni hali iliyosababisha uharibifu wa Mazingira kutokana na ukataji mkubwa wa miti.
Amesisitiza kuwa, matumizi ya Nishati chafu yana athari kubwa kiafya na kimazingira akieleza kwamba, takribani watu milioni 4 hufariki Duniani kila Mwaka kutokana na athari za matumizi ya Nishati chafu.
Ameiagiza STAMICO kupitia Mwenyekiti wa Bodi Mhe: Balozi IGP Mstaafu Simon Sirro, kuhakikisha STAMICO inaendelea kujiendesha kwa ufanisi na kuweza kushindana na Makampuni makubwa ya uchimbaji madini.
Naye Mhe: Subira Mgalu, Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini aliipongeza Wizara kwa mwenendo mzuri waw a Sekta ya Madini kupitia program zake mbalimbali za kuongeza thamani Madini yote yanayochimba Nchini.
Awali akimkaribisha Mgeni Rasmi, Mhe: Upendo Wella, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tabora ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Tabora, alisema Kiwanda hicho kitaleta suluhisho kwa Wakulima wa Tumbaku, Taasisi na watu binafsi.
Tukio hilo la uzinduzi limeenda sambamba na ugawaji wa Vyeti vya uwakala na makontena kwa vikundi vitano vya Wanawake na Samia katika Mikoa ya Tabora, Kigoma, Katavi, Rukwa na Singida. Pia Shirika limesaini Mkataba wa mashirikiano ( Mou ) na Chama kikuu cha Ushirika wa Tumbaku Mkoa wa Tabora ( WETCU ) ili kuwaunganisha vizuri wakulima na STAMICO kutumia Rafiki Briquettes.