STAMICO YAWAPIGA MSASA WATUMISHI WAKE UMUHIMU WA UWAJIBIKAJI KWA MASLAHI YA USALAMA WA NCHI
Shirika la Madini la Taifa ( STAMICO ) limewapatia mafunzo Watumishi wake katika masuala ya uwajibikaji, maadili katika utumishi wa Umma, afya na usimamizi endelevu wa mazingira, jamii na utawala bora ( ESG ).
Mafunzo hayo yametolewa katika kikao cha Wafanyakazi kilichofanyika Aprili 17, 2026 katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania jijini Mwanza kwa lengo la kuwapa uelewa mpana Watumishi hao katika kuongeza ufanisi wao.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse amewaasa Watumishi wa STAMICO kufanya kazi kwa uaminifu, uadilifu, kuheshimiana na kufuata Sheria, kanuni na miongozo ya Serikali ili kuleta matokeo Chanya kwa Shirika na jamii kwa ujumla.
Dkt. Mwasse amesema kuwa, kila mmoja ana dhamana ya kuleta utulivu katika nchi kwa kuwajibika kwa weledi ili kuleta utulivu ndani ya nchi. Aliongeza kuwa, Watanzania sasa wanataka kuona wanavyonufaika na Rasilimali zao.
Ameongeza kuwa, Shirika limetoa fursa hii ili kuwaongeza ujuzi Watumishi wake na kuboresha utendaji wao wa kazi unaoendana na utumiaji wa Rasilimali stahiki katika uendeshaji wa miradi ya Shirika na kusema kuwa Kikao hicho kitatoa mwelekeo wa uendeshaji wa shughuli za Taasisi kwa Mwaka 2026/2027.
Naye Mkurugenzi wa Rasilimali watu na Utawala, Bw. Deusdedith Magala amewasisitiza Watumishi wote kufanya kazi kwa bidi, juhudi na weledi ili kuleta tija kwa Shirika ambalo limejipambanua kujiendesha kwa ufanisi na kujitegemea.
Watumishi wameushukuru Uongozi wa Shirika kwa mafunzo na maadili, afya pamoja na usimamizi endelevu wa mazingira, jamii na utawala bora kwa sababu utawasaidia kuendana na viwango vya Kimataifa.
Awali Watumishi wa STAMICO walipata nafasi ya kutembelea Kiwanda cha kusafisha dhahabu ( Mwanza Precious Metal Refinery ) na kupata mafunzo kuhusiana na mradi huo ambao Shirika lina Ubia na Kampuni kutoka Dubai.
STAMICO inaendelea na azma yake ya kuwapatia mafunzo Watumishi wake ili waweze kufanya kazi kwa weledi na ufanisi.