STAMICO YASHIRIKI MAADHIMISHO SIKU YA WAFANYAKAZI DUNIANI
Wafanyakazi wa Shirika la Madini la Taifa ( STAMICO ) wameungana na wafanyakazi wengine kote Duniani kuadhimisha Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani ( Mei Mosi ) ambapo maadhimisho hayo Kitaifa yamefanyika katika viwanja vya Lunyanywi, Halmashauri ya Mji wa Njombe Mkoani Njombe.
Maadhimisho hayo yalikuwa na kauli mbiu inayosema KAZI ZENYE STAHA NI NGUZO IMARA KWA MAENDELEO ENDELEVU KATIKA UTEKELEZAJI WA DIRA YA TAIFA 2050
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Afisa Rasilimali Watu Mwandamizi wa Stamico, Bi. Leah Jeriko amesema, ushiriki wa STAMICO Kitaifa na kwenye Mikoa ni ishara ya kuthamini mchango wa Wafanyakazi katika maendeleo ya Taifa pamoja na kutambua nafasi zao katika kukuza sekta ya Madini nchini.
Aidha amelishukuru Shirika kwa kuwawezesha Wafanyakazi kushiriki katika maadhimisho hayo Kitaifa na kwenye Mikoa mbalimbali na ametoa wito kwa Watumishi wote kuendelea kufanya kazi kwa bidii, weledi na uzalendo ili kuhakikisha STAMICO inafikia malengo iliyojiwekea.
Kwa upande wake Mfanyakazi Hodari wa STAMICO wa Mwaka huu, Bw. Mark Magesa ameushukuru uongozi wa STAMICO na Watumishi wenzake kwa kumuona anafaa kupata tuzo hiyo na amesema kuwa, kuhudhuria maadhimisho hayo kumewapa fursa ya kujifunza mambo mbalimbali, kubadilishana uzoefu na kujenga mshikamano na Wafanyakazi kutoka Taasisi nyingine.
Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani hufanyika kila Mwaka Mei Mosi kwa lengo la kutambua mchango wa Wafanyakazi katika maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.
STAMICO imeshiriki maadhimisho hayo Kitaifa Mkoani Njombe sambamba na Ofisi zake zote katika Mikoa ya Dar es salaam, Dodoma, Singida, Geita na Songwe.