Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Madini la Taifa

MIRADI YA STAMICO KULETA MAPINDUZI MAKUBWA KIUCHUMI MIKOA YA KUSINI

Imewekwa: 08 May, 2026
MIRADI YA STAMICO KULETA MAPINDUZI MAKUBWA KIUCHUMI MIKOA YA KUSINI

Shirika la Madini la Taifa ( STAMICO ) limeendelea kuimarisha uwekezaji katika sekta ya madini kupitia miradi mikubwa ya Nikeli na Chumvi inayotarajiwa kuongeza ajira, kukuza pato la Taifa na kuinua maisha ya wananchi wa mikoa ya Kusini mwa Tanzania.

Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse, Mei 7, 2026 aliendelea na ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi hiyo mkoani Lindi, ikiwemo mradi wa uchimbaji na uchakataji wa madini wa madini ya Nikeli katika Kijiji cha Nditi, Wilayani Nachingwea.

Katika ziara hiyo, Dkt. Mwasse alitembelea Kiwanda cha kuongeza thamani ya madini ya Nikeli pamoja na mgodi unaoendeshwa kwa ubia kati ya STAMICO na Kampuni ya Coast Nickel.

Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Dkt. Mwasse aliipongeza Kampuni ya Coast Nickel kwa kuanzisha Kiwanda cha kuongeza thamani ya madini ya Nikeli ( Flotation Factory ) chenye uwezo wa kuchakata zaidi ya tani 300 kwa siku, huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza uwezo wa uzalishaji hadi kufikia tani 1,000 na kuendelea kadri shughuli zinavyopanuka.

Aidha alikagua shughuli mbalimbali za uchimbaji, uchakataji pamoja na ghala la kuhifadhi Nikeli kabla ya kusafirishwa.

Dkt. Mwasse pia aliutaka uongozi wa mgodi huo kuendelea kuzingatia masuala ya usalama, afya, mazingira na mafunzo kwa wafanyakazi ili kuhakikisha shughuli za uzalishaji zinafanyika kwa viwango vya kisasa.

Alisisitiza umuhimu wa kuboresha mazingira ya kazi kwa wafanyakazi, ikiwemo makazi, huduma za chakula na maeneo ya burudani, ili kuongeza ufanisi na kuwafanya kudumu kazini.

Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Lindi, Mha. Emmanuel Shija, aliipongeza Kampuni ya Coast Nickel kwa kuendelea kuzalisha na kulipa kodi za Serikali kwa wakati.

Alisema kuwa, Kampuni hiyo inapaswa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya kisasa ya uzalishaji ili kuongeza tija na kuifanya sekta ya madini kuwa na ushindani mkubwa zaidi.

Awali, Dkt. Mwasse alitembelea ghala la kuhifadhi madini ya Nikeli lililopo Vikindu, Mkoani Pwani kabla ya kusafirishwa nje ya nchi.

Sambamba na ziara hiyo, Dkt. Mwasse alikagua maendeleo ya Kiwanda cha kuchakata chumvi kinachojengwa Mkoani Lindi, ambapo usimikaji wa mitambo umefikia asilimia 95.

Kiwanda hicho kinatarajiwa kuchakata zaidi ya tani 24 za chumvi kwa siku na kutoa suluhisho kwa wachimbaji wa chumvi wa Mkoa wa Lindi pamoja na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wakazi wa maeneo jirani.

STAMICO imejipanga kuendelea kuendesha miradi yake kwa ufanisi ili kuchochea maendeleo ya sekta ya madini na Uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo

slot gacor