STAMICO YANG'ARISHA JUKWAA LA LOCAL CONTENT KUONGEZA USHIRIKI WA WATANZANIA KWENYE UVUNAJI MADINI
Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limeendelea kuthibitisha nafasi yake kama Taasisi muhimu katika kukuza sekta ya madini nchini baada ya kuwa mdhamini mkuu wa kipengele cha Gold katika Jukwaa la Local Content linaloendelea kufanyika katika Ukumbi wa Malaika Beach Resort, jijini Mwanza.
Ushiriki wa STAMICO katika jukwaa hilo unaakisi dhamira ya Serikali ya kuhakikisha Watanzania wananufaika zaidi na rasilimali za madini kupitia ushiriki mpana wa wazawa katika mnyororo mzima wa thamani wa sekta hiyo.
Jukwaa hilo limewakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya madini, wawekezaji, watoa huduma, taasisi za serikali na sekta binafsi kwa lengo la kujadili fursa zilizopo na namna ya kuongeza ushiriki wa maudhui ya ndani (Local Content).
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa jukwaa hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse, alisema Shirika limeamua kudhamini jukwaa hilo kwa kutambua umuhimu wake katika kuimarisha ushiriki wa Watanzania katika shughuli za uchimbaji, uongezaji thamani wa madini na utoaji wa huduma mbalimbali zinazohusiana na sekta hiyo.
Alieleza kuwa STAMICO imepiga hatua kubwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, hatua zinazoonyesha mageuzi makubwa ya shirika hilo. Kwa mujibu wa Dkt. Mwasse, mapato ya shirika yameongezeka kwa kiwango kikubwa kutoka takribani shilingi bilioni 1.3 hadi kufikia zaidi ya shilingi bilioni 100 kwa sasa, jambo linalodhihirisha ukuaji wa shughuli za uzalishaji, uwekezaji na usimamizi wa miradi mbalimbali ya madini.
Aidha, alisema STAMICO imeendelea kuwekeza katika teknolojia ya kisasa kwa kuongeza uwezo wake wa kufanya utafiti na uchorongaji wa madini. Alibainisha kuwa kwa sasa shirika linamiliki rigi 18 za kisasa za uchorongaji, huku nyingine sita zikiwa tayari zimeagizwa na zinatarajiwa kuwasili hivi karibuni. Hatua hiyo, alisema, itaongeza ufanisi katika shughuli za utafutaji wa madini na kupunguza utegemezi wa huduma kutoka nje ya nchi.
Mbali na sekta ya madini, Dkt. Mwasse alisema STAMICO imeendelea kutekeleza mkakati wa kuwekeza katika Nishati mbadala kupitia uzalishaji wa Rafiki Briquettes, bidhaa inayolenga kupunguza matumizi ya mkaa na kuni pamoja na kulinda mazingira. Ameabainisha kuwa mwezi ujao Shirika linatarajia kuzindua rasmi Kiwanda kikubwa cha uzalishaji wa Rafiki Briquettes katika Mkoa wa Dodoma, hatua itakayoongeza uzalishaji wa nishati safi na kutoa ajira kwa Watanzania.
Pia alieleza kuwa STAMICO imepanua wigo wa bidhaa zake kwa kuanzisha uzalishaji wa Rafiki Salt, bidhaa mpya inayolenga kukidhi mahitaji ya soko la ndani na kuongeza thamani ya uwekezaji wa shirika katika viwanda.
Dkt. Mwasse aliwahimiza washiriki wote wa Jukwaa la Local Content kutembelea banda la STAMICO ili kujionea mafanikio ya Shirika hilo, kupata elimu kuhusu bidhaa za Rafiki Briquettes na Rafiki Salt, pamoja na kufahamu fursa mbalimbali za uwekezaji na ushirikiano zinazopatikana kupitia STAMICO.
Alisisitiza kuwa STAMICO itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha sekta ya madini inakuwa chachu ya ukuaji wa uchumi wa taifa, huku Watanzania wakipewa kipaumbele katika kunufaika na rasilimali za nchi kupitia sera ya maudhui ya ndani (Local Content). Jukwaa hilo lililoanza tarehe 22 Julai 2026 na Kufunguliwa na Waziri wa Madini,Mhe. Anthony P. Mavunde linatarajiwa kuhitimishwa rasmi tarehe 24 julai 2026