Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Madini la Taifa

STAMICO YASAINI MKATABA WA UENDELEZAJI WA LESENI YA MADINI YA KINYWE NA KAMPUNI YA PLANET ONE YA SINGAPORE

Imewekwa: 30 March, 2026
STAMICO YASAINI MKATABA WA UENDELEZAJI WA LESENI YA MADINI YA KINYWE NA KAMPUNI YA PLANET ONE YA SINGAPORE

Shirika la Madini la Taifa ( STAMICO) katika azma yake ya kuendelea kuvutia wawekezaji wenye tija, leo tarehe 30 Machi, 2026 limesaini Mkataba wa ubia wa kuendeleza leseni zake tatu za Madini ya Kinywe ( Graphite ) na Kampuni kutoka Singapore ya Planet One Natural Resourses Holdings PTE LTD.

Shughuli hiyo ya utiaji saini Mkataba huu imeshuhudiwa na Naibu Waziri wa Madini Mhe. Dkt. Steven Kiruswa.

Akizungumza katika Hafla hiyo, Dkt. Kiruswa amesema kuwa, Mkataba huo ni hatua muhimu itakayochochea maendeleo endelevu katika eneo la Mirerani, Wilaya ya Simanjiro na Mkoa wa Manyara kwa ujumla.

Amesisitiza kuwa, utekelezaji wa mradi huo unapaswa kuwanufaisha Wananchi wa eneo husika kwa kuwapa kipaumbele katika ajira pamoja na kushirikishwa kikamilifu katika shughuli za Kiuchumi zinazotokana na mradi huo.

Aidha amesema kuwa, Madini ya Kinywe ni Madini ya kimkakati yenye mahitaji makubwa Duniani hususani katika utengenezaji wa betri za magari ya umeme, hivyo kutoa fursa adhimu kwa Tanzania Kiuchumi.

Katika hatua nyingine, amezitaka STAMICO pamoja na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania ( GST ) kuendelea kuwasaidia wachimbaji wadogo kwa kuwapatia taarifa sahihi za Kijiolojia ili kuongeza tija katika shughuli zao.

Dkt. Kiruswa amesema kuwa, mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuifanya sekta ya Madini kuwa kichocheo kikuu cha ukuaji wa Uchumi wa Taifa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse amesema, Shirika linaendelea kuvutia uwekezaji mkubwa katika sekta ya Madini huku akibainisha kuwa, huu ni Mkataba wa tatu kusainiwa ndani ya Mwaka huu.

Ameongeza kuwa, mradi huo utachangia kuongeza mapato ya Serikali kupitia fursa mbalimbali zitakazotokana na shughuli zake.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya STAMICO ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Balozi Simon Sirro amesema, uwekezaji huo unaonesha dhamira ya Serikali ya kuimarisha Uchumi wa Wananchi kupitia rasilimali za Madini.

Aidha Balozi Sirro amewataka Wananchi wa Simanjiro kushirikiana na wawekezaji pamoja na kuzingatia uadilifu hasa kwa wale watakaopata fursa za ajira katika mradi huo.

Kwa mujibu wa Balozi Sirro,mapato ya STAMICO yameongezeka kutoka shilingi bilioni 19.81 Mwaka 2021/2022 hadi kufikia shilingi bilioni 72.99 Mwaka 2024/2025, jambo linaloashiria ukuaji wa Shirika hilo.

Kwa upande wake Bw. Ramakrishna Chinnamsetty, Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Planet One amesema, Mkataba huo utaimarisha ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Tanzania na Singapore.

Bw. Chinnamsetty ameongeza kuwa, mradi huo ni zaidi ya uchimbaji wa Madini ya kinywe ( Graphite ) ambao utachochea maendeleo ya miundombinu , afya, elimu na teknolojia. Amesema kuwa, wamejipanga kuheshimu mazingira, utamaduni, na kushirikiana na jamii.

Awali akizungumza katika Hafla hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo alisema kuwa, Wizara inaendelea kusimamia sekta ya Madini kwa kuzingatia Sera , Sheria, na mifumo madhubuti ya kuendeleza utafiti, uchimbaji na uongezaji thamani wa Madini Nchini.

STAMICO inaendelea kujipanga katika mpango wake wa uchimbaji mkubwa kwa kuvutia wawekezaji wenye tija kwa sekta nzima ya Madini.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo