STAMICO KUING'ARISHA STAMIGOLD AJIRA ZAIDI KUZALISHWA
Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limezindua mpango mkubwa wa Upanuzi wa Mgodi wa STAMIGOLD uliopo Biharamulo, Mkoani Kagera, likilenga kuongeza uzalishaji wa dhahabu na kurejesha hadhi ya Mgodi huo katika sekta ya madini nchini.
Akizungumza wakati wa ziara ya Bodi ya Wakurugenzi wa STAMICO, Meneja Mkuu wa STAMIGOLD, Mha. Ally Saidy, amesema Kampuni hiyo imejipanga kuanza uzalishaji mkubwa unaotarajiwa kufikia zaidi ya Wakia 78,439.9 za dhahabu ifikapo mwaka 2031, kufuatia uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanyika mgodini hapo.
Mpango huo wa upanuzi unahusisha ununuzi wa mitambo ya kisasa ya uchorongaji na utafiti wa madini, maboresho na upanuzi wa mitambo ya uchakataji pamoja na mfumo wa elution, sambamba na uwekezaji katika magari, mitambo mizito na matingatinga ( Bulldozer )ya kubeba udongo ili kuongeza uwezo wa uzalishaji.
Mha. Saidy aliongeza kuwa mradi huo unatarajiwa kuongeza nafasi za ajira zaidi ya wafanyakazi 700 waliiopo sasa,huku ajira nyingine zikitarajiwa kuongezeka katika mwaka wa fedha 2026/2027.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse, amesema Taasisi ya Jiolojia Tanzania (GST) wapo tayari kuunga mkono tafiti za kina za uchimbaji zitakazosaidia kubaini maeneo mapya ya madini na kuhakikisha uzalishaji endelevu wa dhahabu kwa muda mrefu.
Aidha, Bodi ya Wakurugenzi ya STAMICO imeidhinisha mipango kazi ya STAMIGOLD kwa mwaka 2026/2027 na kusisitiza utekelezaji wake wa haraka ili kufikia malengo ya uzalishaji, kuongeza ajira kwa Watanzania na kukuza mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa taifa.
STAMICO inaendelea na uwekezaji kwenye miradi yake ya madini kama sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kutumia rasilimali za madini kufaidisha vizazi vya sasa na vijavyo.