Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

State Mining Corporation

State Mining Corporation

News

STAMICO YATINGA PEMBA KUTOA ELIMU YA NISHATI YA KUPIKIA YA RAFIKI BRIQUETTE


Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limepongezwa kwa juhudi zake za kuendelea kutoa elimu ya matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia ya Rafiki Briquette.

Pongezi hizo zimetolewa leo tarehe 31 Oktoba,2024 na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,Mhe. Hemed Suleiman Abdullah wakati akifunga Kongamano la Kumpongeza Rais wa Zanzibar,Mhe,Dkt. Hussein Mwinyi ambalo limefanyika kwenye Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi,Wete,Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Amesema Serikali ya Zanzibar inatambua mchango mkubwa unaotolewa na wadau mbalimbali kwa jamii ikiwemo STAMICO.

"Kuhifadhi mazingira yetu ni kitu muhimu sana,hivyo nawapongeza wote mliofanikisha kongamano hili.Nimejulishwa pia juhudi za STAMICO kuendelea kutoa elimu ya matumizi ya nishati hii.Nawashukuruni sana"alisema.

Kongamano hilo smbalo limehudhuriwa na washiriki zaidi ya 800 limeandaliwa na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT).

Awali,Makamu Mwenyekiti wa UWT Taifa,Mhe.Zainab Shomari ameupongeza uongozi wa STAMICO kwa mchango wake kufanikisha kongamano hilo.

Amesema kuwa kisiwa cha Pemba kinakabiliwa na athari za ukataji miti na matumizi ya mkaa na kuni,hivyo nishati ya Rafiki Briquette itakuwa suluhisho la kudumu la changamoto hiyo.

Ameahidi kuwa UWT itakuwa balozi mzuri wa nishati ya Rafiki Briquette nchini kote.

Mratibu wa Mradi wa Rafiki Briquette,Mha.Happy Mbenyange ametoa taarifa fupi kuhusu nishati hiyo ambayo imewavutia washiriki wa kongamano hilo.

Kabla ya tukio la leo katika muendelezo wa shughuli za maadhimisho ya miaka minne ya Rais Mwinyi tangu aingie madarakani,STAMICO pia ilitoa elimu ya matumizi ya nishati ya Rafiki Briquette wakati wa uzinduzi wa masoko ya kisasa ya Mwanakwerekwe na Jumbi,Mkoa wa Magharibi,Unguja tarehe 26 na 27 Oktoba 2024.

Rais Dk.Mwinyi pia alivutiwa na nishati hii alipofungua masoko hayo.

STAMICO ilishiriki kwenye uzinduzi wa masoko haya mawili kwa kuonesha kwa vitendo namna ya kupika kwa kutumia nishati hii ambayo imekuwa inajipatia umaarufu katika maeneo mengi hapa nchini.

STAMICO ilialikwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuonesha namna ya kutumia nishati hii kwa mama na baba lishe 150 kwenye masoko haya mawili.

Wiki tatu zilizopita,nishati hii ilivutia wananchi wengi wakati wa maonesho ya Madini yaliyofanyika mkoani Geita.