Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

State Mining Corporation

State Mining Corporation

News

STAMICO YAWAKUTANISHA WADAU MUHIMU USAFIRISHAJI DHAHABU NJE YA NCHI MWANZA


Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwa kushirikiana na Mwanza Precious Metals Refinery (MPMR) limewakutanisha wadau wa usafirishaji wa dhahabu nje ya nchi kwa lengo la kujadiliana changamoto zilizopo katika usafirishaji wa dhahabu hususan unaofanywa na Kiwanda hicho chenye hadhi ya kimataifa. Kikao cha kuwakutanisha wadau hao kilifanyika tarehe 13 Julai, 2023 jijini Mwanza na kiliongozwa na Mkurugenzi Mtendaji STAMICO, Dkt. Venance Mwasse.

Wadau waliokutanishwa ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Tume ya Madini, Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) na IMAWORX Tanzania Limited.

Katika Kikao hiki changamoto ya ucheleweshaji wa zoezi la usafirishaji wa dhahabu iliyosafishwa (refined gold) nje ya nchi zilijadiliwa na kupata majibu lengo likiwa kuongeza tija na manufaa kupitia uwepo wa kiwanda cha Mwanza Precious Metals Refinery ambao ni uwekezaji wa ubia kati ya STAMICO na wawekezaji kutoka Dubai.

Akiwasilisha changamoto katika usafirishaji wa dhahabu nje ya nchi Bw. Deusdedith Magala , Mwenyekiti Kamati ya Uendeshaji ya Pamoja (JMC) alisema kumekuwa na ucheleweshaji kwanza kwenye ufungaji (boxing) wa dhahabu ilisafishwa na pia mlolongo mrefu wakati kusafirisha nje ya nchi. Hali hii inaleta usumbufu sana kwa kampuni.

Kwa upande TRA, Bw. Adeus Fransic mwakilishi wa Meneja Mkoa wa Mwanza alisema kama TRA wako tayari kufanya kazi usiku na mchana ili uwekezaji huu wa kiwanda hiki uwe na tija kwa nchi na kwa mwekezaji. Aidha Bw. Fransis aliahidi kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu changamoto zote zinazokwamisha zoezi kwani Serikali inahamasisha uwekezaji wa mitaji kutoka ndani na nje ya nchi kwa manufaa ya Tanzania.

Dkt. Mwasse alisisitiza kuhakikisha kuwa mikakati iliyowekwa kutokana na kikao hicho iongeze kasi na kuhakikisha zoezi la ufungaji wa dhahabu iliyosafishwa na taratibu za usafirishwaji wake unafanyika ndani ya siku moja ili dhahabu isafirishwe nje ya nchi kwa wakati.