UFANISI WA STAMICO CHACHU KWA MAENDELEO YA UCHUMI
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Bw. Msafiri Mbibo amelipongeza Shirika la Madini la Taifa ( STAMICO ) kwa jitihada zinazofanywa na Uongozi na Watumishi wake katika kuchangia ukuaji wa Uchumi wa nchi.
Pongezi hizo amezitoa wakati akizindua Baraza la tatu la Wafanyakazi wa STAMICO lililofanyika Aprili 18, 2026 katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania jijini Mwanza.
Akiongea kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Bw. Mbibo ametoa rai kwa wajumbe hao wa Baraza kuwa mfano wa kuigwa katika uwajibikaji, uadilifu na weledi.
Amesisitiza pia kuendelea kujengwa kwa utamaduni wa mawasiliano mazuri kati ya Viongozi na Watumishi, ushirikishwaji wa Watumishi katika utekelezwaji wa shughuli za Shirika huku akiielekeaza Menejimenti kushughulikia changamoto za Watumishi kwa wakati ili waweze kufanya kazi kwa bidii na kufikia malengo ya Shirika na Serikali kwa ujumla.
Amesema kuwa,Wizara itaendelea kushirikiana na STAMICO katika kutatua migogoro na changamoto zitakazojitokeza katika utekelezaji wa majukumu na uendeshaji wa shughuli zake.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse ambaye ndiye Mwenyekiti wa Baraza hilo, amewaahidi Wajumbe wa Baraza hilo kuendelea kuboresha maslahi ya Watumishi kadri Shirika litakavyokuwa likiendelea kufanya vizuri.
Dkt. Mwasse ameongeza kuwa, suala la maslahi bora kwa Watumishi ni kipaumbele chake kikubwa na kadri Shirika litapofanya vizuri na maslahi ya Watumishi yatazidi kuwa mazuri.
Akizungumza katika Kikao hicho, mwakilishi wa Msajili wa Hazina Bw. Chacha Marigiri , amesema STAMICO ni miongoni mwa mashirika ambayo yanafanya vizuri ambapo ni ndoto ya Msajili wa Hazina kuona STAMICO inashindana Kimataifa.
Aidha katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi TAMICO, Bw. Peternus Rwechungura ameipongeza STAMICO kwa kujali matakwa ya kisheria yanayowahusu Watumishi.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi TAMICO, Bw. Vitus Chaniko amemshukuru Dkt. Mwasse kwa uongozi thabiti ambao umeleta matokeo chanya lakini pia katika kuendelea kuboresha maslahi ya Watumishi.
STAMICO inaendelea kujipambanua kama Shirika linalojali maslahi ya Watumishi wake kwa kujenga mazingira bora ya kufanya kazi kwa ufanisi.