Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Madini la Taifa

KAMATI YA BUNGE YA KUDUMU YA NISHATI NA MADINI YAIPA HEKO STAMICO KWA UFANISI KWENYE KUIONGEZEA THAMANI DHAHABU NCHINI

Imewekwa: 03 May, 2026
KAMATI YA BUNGE YA KUDUMU YA NISHATI NA MADINI YAIPA HEKO STAMICO KWA UFANISI KWENYE KUIONGEZEA THAMANI DHAHABU NCHINI

Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Nishati Madini imefanya ziara ya kukagua Kiwanda cha kusafisha dhahabu cha Mwanza Precious Metal Refinery ( MPMR ) kilichopo Wilayani Ilemela Mkoani Mwanza, ambacho kinamilikiwa kwa Ubia kati ya STAMICO na Kampuni ya Goodfield kutoka Falme za Kiarabu.

Katika ziara hiyo kamati imeridhishwa na utendaji wa kiwanda hicho na imeipongeza STAMICO  kwa kusimamia maslahi ya Serikali kwa kuhakikisha dhahabu inayochimbwa inaongezwa thamani kabla haijatoka nchini kama sheria zinavyosema.

Pongezi hizo zimetolewa na  Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya kudumu Mhe. Subira Mgalu katika ziara hiyo iliyofanyika tarehe 02/05/2026, ambapo amesema kuwa, Sekta ya Madini ni Sekta inayofanya vizuri katika kuchangia pato la Taifa na ni Sekta ya kimkakati katika utekelezwaji wa Dira 2050 kufikia Uchumi wa trillioni moja.

Amesema kwamba, wao kama Wabunge wamefurahishwa kuona kwa vitendo jinsi Serikali kupitia STAMICO na Kampuni hii ya Ubia ambavyo wameweza kuja na mradi huu ambao unaongeza thamani kwenye madini ya dhahabu na hivyo kuongeza mapato kwa Nchi.

Ameeleza kuwa, Wananchi wa Ilemela na maeneo ya jirani wapate kipaumbele katika mpango wa ushirikishwaji wa jamii inayozunguka eneo la mradi ( Local Content ) pamoja na mpango wa kurudisha kwa jamii ( CSR ).

Naye Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema kuwa, Wizara imeanza mchakato wa kuwatambua wachimbaji na wafanyabiashara wa madini ili wawe na uwezo wa kupata fedha kupitia Serikali kwa minajili ya kupunguza utegemezi wa kupeleka mzigo wa dhahabu Dubai.

Mhe. Mavunde amefafanua kuwa, Wizara inataka kuhakikisha shughuli zote zifanyike nchini kitu kitakachowezesha wafanyabiashara kuwa na uwezo wa kuufuata mzigo nchini Tanzania badala ya kulazimika kwenda Dubai, jambo ambalo litawapunguzia gharama lakini litaongeza mapato kwa nchi.

Amemalizia kwa kutoa maelekezo kwa STAMICO kuhakikisha wanayatekeleza maagizo ya kamati kwenye mpango wa CSR na Local Content.

Awali akifanya wasilisho la STAMICO kwa kamati hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse amesema kuwa, Kiwanda hicho cha kusafisha dhahabu kina uwezo wa kusafisha kilo 480 kwa siku katika kiwango cha Kimataifa cha ubora wa 999.9/% ambao ni ubora unaoifanya dhahabu kuwa kwenye viwango vya uhifadhi wa fedha ( Currency ). Kutokana na uwezo huu, kiwango kikubwa kinachozalishwa kinauzwa kwa Benki kuu ya Tanzania na Kiwanda hicho kimeiwezesha Benki kuu ya Tanzania kuwa na uhifadhi mzuri wa dhahabu ambao unatumika kulinda hifadhi ya fedha za nchi.

Ameongeza kuwa, Kiwanda hicho kimeongeza mapato ya nchi kupitia mrabaha, kimeongeza mapato kwa Shirika  na kuifanya dhahabu iliyozalishwa Tanzania kutambulika na kuwa na nembo yake maalum.

Dkt. Venance Mwasse amebainisha kuwa, STAMICO inaendelea kushughulikia changamoto ya upatikanaji wa malighafi kwa kuendelea kuwawezesha wachimbaji na makampuni katika shughuli za uchimbaji ili kuongeza uzalishaji kwa utaratibu wa advance payment.

Naye Mkuu wa Wilaya ya  Nyamagana Bi. Amina Makilagi akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ameiomba STAMICO kuhakikisha wakazi wa Wilaya ya Ilemela wananufaika na uwepo wa Kiwanda hicho.

STAMICO inaendelea na azma yake ya kusimamia Rasilimali zote za madini ambazo imekasimishwa na Serikali kwa ufanisi ili kuleta tija kwa nchi na kuongeza mapato ya madini kwa nchi.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo