Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Madini la Taifa

SERIKALI YAWAFIKIA WACHIMBAJI MVOMERO

Imewekwa: 19 January, 2026
SERIKALI YAWAFIKIA WACHIMBAJI MVOMERO

MD STAMICO aongoza timu ya wataalamu

Aahidi kutengeneza mabilionea katika sekta ya Madini

Vijana wahimizwa kujitokeza kuchangamkia fursa

Diwani na Wachimbaji waishukuru Serikali.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Dkt. Venance Mwasse amefanya ziara kutembelea migodi ya wachimbaji wadogo iliyopo kata ya Kibata Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro leo tarehe 17/01/2026. Akiambatana na na timu ya wataalamu Mkurugenzi Mtendaji amefika kujionea shughuli za uchimbaji katika eneo hilo na alipata wasaa wa kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili wachimbaji.

Akieleza kuhusu changamoto zilizopo Diwani wa Kata hiyo  Mhe. Costa Peter Reuben ameishukuru Serikali kwa kuwakumbuka na kusema kuwa, wachimbaji wa machimbo ya Kibati wanakabiliwa na ukosefu wa vitendea kazi, huduma za utafiti pamoja na ukosefu wa mitaji.

Pamoja na changamoto hizo Mhe. Diwani ameongeza kuwa, suala la ukosefu wa usalama mahali pa kazi ni tatizo kubwa kwa migodi mingi iliyopo katika eneo hilo.

Akiongea na wachimbaji , Dkt. Mwasse amesema kuwa Serikali imesikia kilio cha wachimbaji na imejipanga kuwasaidia kutatua changamoto zinazowakabili.

kwa kuanzia Dkt. Mwasse amesema kuwa STAMICO itawapelekea mtambo wa uchorongaji na wataalamu ili waweze kubaini mashapo yalipo ili wasichimbe kwa kubahatisha tena.

Aidha , Dkt. Mwasse ameongeza kuwa STAMICO itafanya mafunzo juu ya teknolojia rahisi ya uchenjuaji dhahabu na kuendesha mafunzo juu ya usalama migodini. Lengo Serikali kupitia STAMICO ni kuboresha na kuongeza uwezo wa wachimbaji wazawa ili kuongeza mchango wao kwenye pato la Taifa.

STAMICO imedhamiria kutengeneza Mabilionea vijana kupitia sekta ya Madini, hivyo ni jukumu lenu kuchangamkia fursa zinazotengenezwa na STAMICO, amesema Dkt. Mwasse.

Akichangia katika majadiliano hayo, Meneja Utafiti wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Ndg, Fredrick Mangasini amewahimiza wachimbaji wadogo kuendelea kutumia huduma za kitaalamu zinazotolewa na STAMICO kwani Shirika lina wataalamu wabobezi kwenye mnyororo mzima wa thamani wa Madini. Nae Mjiolojia Mkuu wa STAMICO Ndg, Alex Rutagwelela ameongeza kuwa, STAMICO ina mitambo ya kisasa ya uchorongaji na vifaa vya utafiti wa Kijiofizikia vilivyonunuliwa mahsusi kwa ajili wa wachimbaji wadogo. Hivyo Shirika linawakaribisha wachimbaji kunufaika na utafiti kwa kutumia mitambo na vifaa hivi.

Akishukuru kwa niaba ya wachimbaji wenzake Ndg, Sylvester Sayi amesema kuwa, ujio wa Mkurugenzi Mtendaji STAMICO na timu ya wataalamu katika migodi yao ni uthibitisho kamili wa namna STAMICO inavyowathamini wachimbaji wadogo. Aidha Ndg, Sayi ameongeza kuwa wao kama wachimbaji wazawa wanapokea kwa mikono miwili msaada wa kitaalamu utakaoletwa na STAMICO kuahidi kutoa ushirikiano wote utakaohitajika.

Katika ziara hiyo Mkurugenzi Mtendaji aliambatana na Meneja anayeshughulikia utafiti Ndg, Fredrick Mangasini, Mjiolojia Mkuu Ndg, Alex Rutagwelela na wajiolojia kutoka Kurugenzi ya Uchorongaji na Utafiti Bi. Happiness Njela na Bi. Lucia Kimaro.

 

 

Mrejesho, Malalamiko au Wazo