News
KIWANDA KIKUBWA CHA KUCHAKATA MADINI YA KIMKAKATI KUANZISHWA TANZANIA
●Ni wabia wa STAMICO, waridhishwa na mazingira Bora ya uwekezaji nchini
●MD STAMICO ashuhudia Teknolojia ya kisasa ya uchakataji wa madini ya kimkakakti
●Ujenzi wa Kiwanda kukamilika na kuanza kazi mwaka huu
*CHINA*
Shirika la Madini la Taifa, kwa kushirikiana na Kampuni ya Coast Nickel Limited linatarajia kuanza ujenzi wa viwanda vikubwa na vya kisasa vya kuchenjua na kuchakata madini ya Nikeli na Shaba nchini Tanzania na kuanza kazi kabla ya kuisha mwaka huu wa 2025
Tayari kontena 24 kati ya 38 zilizolipiwa zimeshaingia nchini.
Mpango huu wa muda mrefu unalenga kuendeleza mradi wake wa uchimbaji mkubwa na uchakataji wa madini haya ya kimkakati yaliyoko katika kilima cha Ntaka, Wilayani Nachingwea, Mkoani Lindi.
Makubaliano hayo yalifikiwa katika katika ziara ya Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa Dkt Venance Bahati Mwasse alipotembelea na kuona shughuli za uchenjuaji na uchakataji madini haya ya kimkakati katika viwanda hivi kati ya tarehe 5 na 8, mwezi Agosti, nchini China. Katika ziara hii Mkurugenzi Mtendaji aliambatana mtaalam wa jiolojia Bw.Alex Rutagwelela na mtaalam wa uhandisi wa migodi na uchenjuaji Mha.Ibrahim Dauda.
Kampuni ya Coast Nickel Ltd ni kampuni tanzu ya Kampuni ya NINGBO SHUANGNENG GROUP inayomiliki mitambo ya aina hii katika miji ya Ningbo,Jimbo la Zhejiang na Mji wa Yangstan, Jimbo la Jiangxi, nchini China.
Awali,Dkt Mwasse na timu yake waliweza kutembelea kiwanda cha Ningbo Shuangneng Environmental Protection Technology ambacho ni kampuni tanzu ya NINGBO SHUANGNENG GROUP. Kiwanda hiki kinachenjua mabaki ya taka (waste/tailings) zinazozalishwa na viwanda mbalimbali vya metali na mafuta (oil & gas)nchini China.
Uongozi wa kiwanda hiki ulilieza Shirika kwamba mkakati huu ni mahususi wa ajili ya uhifadhi na utunzaji mazingira kwa kutumia taka zinazozalishwa na viwanda mbalimbali ambapo kampuni hii huzikusanya kutoka katika maeneo mbalimbali ya China na kuzichakata (recycling) na kuweza kuzalisha madini ya metali mbalimbali yaliyomo katika taka hizi yakiwemo _Lithium,Nickel_ na _Molybdenum_.
Katika vikao vya pamoja,Mkuruzenzi Mtendaji wa Shirika pamoja na wataalam wake walikutana na uongozi wa kampuni ya NINGBO SHUANGNENG GROUP uliokuwa chini ya Mwenyekiti wake Bw Hou Tianyou.
Katika vikao hivyo, Dkt.Mwasse aliwahakikishia wawekezaji hao kwamba, STAMICO ipo tayari kushirikiana na wawekezaji hao katika kuendeleza mradi wa Nikeli, Ntaka, Nachingwea kwa kuhakikisha Shirika linakamilisha kuchambua na kutathmini taarifa za kijiolojia na mashapo ya madini ya Nikeli katika eneo ya leseni ya mradi huu.
Aliongeza kwamba kazi hii itahusisha ukusanyaji wa taarifa za nyongeza za kijiolojia na kusaini kwa leseni eneo ambalo awali lilikuwa halijafanyiwa utafiti wa kina.
Katika hatua nyingine,Dkt.Mwasse aliwahakikishia wawekezaji hao kwamba Shirika litafanya uhakiki huu wa kijiolojia kwa weledi mkubwa ikiwemo kupeleka mtambo mmoja kwa ajili ya kuhakiki taarifa za uchorongaji zilizopo yaani _drilling data validation_ ambapo hatua hii itaenda sambamba na ukadiriaji upya wa mashapo ya Nikeli na Shaba.
Kwa upande wao,wamiliki wa Kampuni ya NINGBO SHUANGNENG GROUP wamesema wako tayari kifedha na kiteknolojia kuja na kuanza mara moja ujenzi wa viwanda hivi nchini Tanzania ili shughuli za uchimbaji, uchenjuaji na uongezaji thamani wa madini haya uanze mara moja.
Aidha,waliliomba Shirika kuharakisha kazi ya uhakiki wa taarifa za kijiolojia na mashapo kwani taarifa hizo ndizo zitaamua ukubwa wa viwanda vitakavyojengwa pamoja na uhai wa viwanda hivi vya madini ya kimkakati.
Katika kuhitimisha ziara hii,Dkt Mwasse amewashukuru wawekezaji hawa kwa mwaliko wa ziara hii ambayo imewezesha STAMICO kuona uwezo wa kiuwekezaji kifedha na ki teknolojia unaofanywa na kampuni ya NINGBO SHUANGNENG GROUP .Aliongeza kwamba ukamilifu wa ujenzi wa viwanda hivi chini kwa ubia na STAMICO utakuwa pia na manufaa kwa wachimbaji wadogo nchini ambao wanajihuaisha na shughuli za uchimbaji madini haya ya kimkakati lakini wanakwama kimasoko kwa kutokuwepo kwa soko la uhakika la madini wanayochimba.
Aidha,Mkurugenzi Mtendaji,alimalizia kwa kuwakaribisha wawekezaji hawa kutembelea Tanzania muda wowote kuanzia sasa ili kubaini fursa zaidi za ushirikiano baina ya Taasisi hizi mbili.