KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA NISHATI NA MADINI YAFURAHISHWA NA TEKNOLOJIA YA UCHENJUWAJI WA DHAHABU KATIKA KITUO CHA MFANO CHA KATENTE
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wameonyesha kuridhishwa na kufurahishwa na kasi ya teknolojia inayotumika katika Kituo cha mfano cha uchenjuwaji Dhahabu cha Katente, kinachoendeshwa na STAMICO katika Wilaya ya Bukombe, Mkoani Geita.
Hayo yamebainishwa leo Machi 15, 2026 na Mhe. Subira Mgalu, Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua maendeleo ya Kituo cha mfano cha Katente .
Mhe. Mgalu ameeleza kuwa, Kamati imefurahishwa na teknolojia ya kisasa ya uchenjuwaji Dhahabu inayotumika katika Kituo cha Katente ya Vat Leaching ambayo imefanikiwa kuongeza kiwango cha upatikanaji wa Dhahabu kutoka asilimia 40 hadi kufikia zaidi ya asilimia 90.
Pia ameipongeza STAMICO kwa kurahisisha upatikanaji wa kemikali, vilipuzi na huduma nyingine zinazoendana na uchimbaji mdogo kwa wachimbaji wadogo wapatao 1019 kupitia Kituo hicho.
Sambamba na hilo Mhe. Mgalu ameipongeza Serikali kwa kusogeza huduma kwa wachimbaji wadogo kupitia Kituo cha Katente, hatua hii inawasaidia wachimbaji wadogo katika kuongeza tija kwenye shughuli zao za uchimbaji.
Kwa upande wake, Mhe. Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa ameishukuru Kamati ya Bunge kwa ushauri mzuri kuhusu kuboresha Kituo hicho ili kuendana na idadi ya wachimbaji wadogo katika kuwapatia huduma.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za uchenjuwaji katika Kituo hicho, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Ndg, Deusdedith Magala amesema kuwa, katika kipindi cha kuanzia Mwaka 2020 hadi Januari 2026, wachimbaji wadogo wapatao 1920 wamepata Elimu juu ya uchimbaji, usagaji mbale, uchenjuwaji na ukamatishaji Dhahabu.
STAMICO inaendelea kutekeleza jukumu lake la kuwalea wachimbaji wadogo kutumia teknolojia itakayosaidia kufanya uchimbaji uwe salama na wenye uhakika.