UWT TAIFA YAIPONGEZA STAMICO KATIKA KUHAMASISHA MATUMIZI YA NISHATI SAFI
Uongozi wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Taifa, ukiongozwa na Mwenyekiti wake, Cde Mary Chatanda (MCC) leo Julai 21, 2026, umetembelea Kiwanda cha Nishati Safi cha Rafiki Briquettes, kinachomilikiwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), kilichopo katika Wilaya ya Kisarawe, Mkoani Pwani.
Katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa UWT Taifa aliongozana na wajumbe wa kamati ya utekelezaji kwa lengo la kujifunza zaidi kuhusiana na Nishati hii kuanzia kwenye uzalishaji mpaka kwenye matumizi ya mtu mmoja mmoja.
Akitoa maelezo kwa viongozi hao, Mhandisi Goodluck Mhagama alisema kiwanda hicho kimejikita katika kuzalisha Nishati Safi yenye ubora wa hali ya juu ambayo ni mbadala wa kuni na mkaa.
Amefafanua kuwa matumizi ya Rafiki Briquettes yanachangia kupunguza ukataji wa miti, kuhifadhi misitu, kupunguza uchafuzi wa mazingira na kusaidia juhudi za Taifa za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, alisema Briquettes zinazozalishwa na STAMICO hudumu kwa muda mrefu wakati wa matumizi, hutoa joto la kutosha kwa shughuli mbalimbali za kupikia na huzalisha moshi na majivu kwa kiwango kidogo ikilinganishwa na nishati za jadi.
Aliongeza kuwa kutokana na ubora wake, bidhaa hiyo imeendelea kupata soko na kukubalika kwa watumiaji wa majumbani na taasisi.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt Venance Mwasse
Ameushukuru Uongozi wa UWT Taifa kwa kutenga muda kuja kutembelea Kiwanda hiki cha Rafiki Briquettes ambacho kinaendana na utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi kuhusiana na matumizi ya Nishati Safi pamoja na Agenda ya Serikali ya Awamu ya Sita yenye mpango wa kuhakikisha Watanzania asilimia 80 wanatoka kwenye matumizi ya Nishati zisizo Safi na kuhamia kwenye Nishati Safi kufikia mwaka 2034.
Ameongeza ujio wa viongozi hao unaonesha namna taasisi mbalimbali zinavyoendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha wananchi wanapata Nishati Safi, salama na yenye gharama nafuu.
Ameleza kuwa STAMICO imeendelea kutekeleza kwa vitendo ajenda ya Nishati Safi kupitia uwekezaji katika uzalishaji wa Rafiki Briquettes, bidhaa ambayo inalenga kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, kuhifadhi mazingira na kuboresha afya za wananchi.
Aidha, amesistiza kuwa ushirikiano kati ya STAMICO na UWT utasaidia kuongeza uelewa wa jamii kuhusu faida za matumizi ya Nishati Safi na ameahidi kutoa ushirikiano kwa UWT itakapokuwa na shughuli za uhamasishaji wa Matumizi ya Nishati Safi.
Kwa upande wake, Mgeni rasmi Mwenyekiti wa UWT Taifa, Bi. Mary Chatanda( MCC) ameipongeza STAMICO kwa ubunifu na jitihada zake katika kuanzisha na kuendeleza uzalishaji wa Rafiki Briquettes.
Ameeleza kuwa STAMICO imeonesha kwa vitendo namna taasisi za umma zinavyoweza kutekeleza maelekezo ya Serikali kuhusu matumizi ya Nishati Safi.
Amesema baada ya kupata mafunzo kuhusiana na Nishati hii ya Rafiki Briquettes, amevutiwa nayo na atahakikisha anaishirikisha STAMICO katika shughuli za UWT ili waweze kuwafikia Wanawake wengi katika uhamasishaji huu wa Nishati Safi.
"Leo tumeshuhudia kwa macho yetu kazi kubwa inayofanywa na STAMICO. Huu ni uwekezaji wenye manufaa makubwa kwa Taifa kwa sababu unalinda mazingira, unalinda afya za wananchi kwa kutoa suluhisho sahihi kwenye matumizi ya Nishati Safi" amesema Mhe Chatanda.
STAMICO inaendelea kuhakikisha kupitia mradi wake wa Rafiki Briquettes inaendelea kuhamasisha matumizi ya Nishati safi kama sehemu ya tekelezaji wa maelekezo ya Serikali kuhusiana na Matumizi ya Nishati Safi kwa Watanzania