STAMICO YATOA ELIMU YA NISHATI SAFI YA RAFIKI BRIQUETTES KWA CHUO CHA MAFUNZO ZANZIBAR
Shirika la Madini la Taifa ( STAMICO) katika maandalizi ya kuanza kuisambaza Nishati Safi ya kupikia ya Rafiki Briquettes katika Vyuo vyote vya mafunzo vya Zanzibar, imetoa mafunzo kwa Viongozi na Maafisa wa Vyuo vya Mafunzo kutoka Zanzibar.
Mafunzo hayo ya kuongeza uelewa kuhusiana na Nishati ya Rafiki Briquettes, yametolewa leo tarehe 21 Agosti 20026 katika Kiwanda cha kuzalisha Rafiki Briquettes cha Kisarawe na kuhudhuriwa na Maafisa na Viongozi kutoka Chuo cha Mafunzo walioongozwa na SSP Khamis Ramadhani.
Akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse, Mkurugenzi wa Migodi na Huduma za Kihandisi STAMICO Mha. Baraka Manyama amewaeleza Maafisa na Viongozi hao mpango wa STAMICO wa kuisambaza Nishati hii katika kisiwa chote cha Zanzibar.
"STAMICO tayari ina viwanda vikubwa vinne vyenye uwezo wa kuzalisha tani 20 kwa saa na ina mpango wa kufungua viwanda vingine zaidi ikiwa ni pamoja na Kiwanda katika Mkoa wa Geita ambacho usimikaji wake utaanza muda mfupi na katika mantiki hiyo Shirika limejipanga kutanua masoko ya Nishati hii nchi nzima" amesema Eng Manyama.
Akitoa mafunzo ya Nishati hii mbele ya maafisa hao, Msimamizi wa Kiwanda hicho cha Rafiki Briquettes, Mha. Goodluck Mhagama amewaelezea Maafisa na Viongozi hao juu ya ufanisi wa Nishati hii kwenye matumizi na uwezo wa kuwaka muda mrefu.
Naye, Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mahusiano kwa Umma, Bw. Deus Alex Ntukamazina amewahakikishia Maafisa hao azma ya STAMICO katika kuhakikisha Nishati hii ya Rafiki Briquettes inawafikia ndani ya Wiki mbili kupitia wakala wake Taasisi ya FDH.
Akiongea kwa niaba ya Maafisa hao, Mgeni Rasmi Afande Ramadhani ameishukuru STAMICO kwa makaribisho mazuri pamoja na mafunzo waliyoyapokea na amesema Maafisa waliopokea mafunzo haya wataenda kuwafunza wengine waliobaki kuhakikisha wana uelewa mzuri kabla ya kuanza kutumia Nishati hii.
STAMICO imejipanga kuhakikisha inaendelea kuwa kinara katika kuhamasisha matumizi ya Nishati safi ya kupikia Tanzania Nzima.