News
STAMICO YAZIDI KUNG'ARA KWENYE CEO's FORUM JIJINI ARUSHA
▪️Yanyakuwa Tuzo ya Shirika lenye ufanisi bora kifedha
▪️Ni mara ya tatu Mfululizo tangia 2023
▪️Katibu Mkuu, Wizara ya Madini naye atambuliwa kwa Tuzo kutokana na Ufanisi huo
Arusha, Agosti 24 2025
Shirika la Madini la Taifa ( STAMICO), limepokea Tuzo kwa ufanisi wake kwenye mapato, matumizi na uwezo wake wa kurejesha gawio la faida Serikalini.
Tuzo hiyo imetolewa leo tarehe 24 Agosti 2025 na Mheshimiwa Dkt Philip Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Mashirika ya Umma .
Kikao kazi hiki huandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina na kinafanyika kila mwaka Jijini Arusha
Kwa mwaka huu kikao hiki kinafanyika katika Ukumbi wa AICC kwa siku nne na kimeanza tarehe 23 Agosti na kitamalizika tarehe 26 Agosti 2025.
STAMICO imetambuliwa katika Taasisi za Umma zinazofanya biashara na zenye ufanisi kwenye maeneo ya mapato, matumizi na uwezo wa kurejesha gawio la faida Serikalini.
Tuzo hii ni miongoni mwa Tuzo tatu ambazo STAMICO imepata kwa miaka mitatu mfululizo
katika vikao kazi hivi vinavyofanyika kila mwaka
Katika hotuba yake Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt Philip Mpango ambaye alikuwa Mgeni Rasmi kwenye ufunguzi wa kikao hiki leo, ameitaja STAMICO kuwa miongoni mwa Taasisi ambazo zimejiondoa katika utegemezi wa Serikali na kuweza kujiendesha kwa faida.
STAMICO imeweza kutoa jumla ya Shillingi Billion kumi (10) kama gawio kutokana na faida ambayo Shirika limetengeneza
Aidha katika kikao kazi hiki Wizara ya Madini pia ilipata tuzo kutokana na ufanisi huo wa STAMICO