News
WABUNGE WAIPONGEZA SERIKALI KWA KUANZISHA VITUO VYA MFANO KWA WACHIMBAJI WADOGO NA KUSISITZA KUENDELEA KUVIIMARISHA
Jana Siku ya Ijumaa Tarehe 14/03/2025 Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ilitembelea eneo la Kituo cha Mfano kwa Wachimbaji Wadogo cha Itumbi kama sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake. Kamati hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti Mhe. Mathayo D. Mathayo (MB) iliambatana na Naibu Waziri wa Madini (NWM) Mhe. Dkt. Steven L. Kiruswa (MB). Katika ziara hiyo, wajumbe wa kamati walitembelea mitambo ya uchenjuaji madini kwa njia za CIP na Elution; na bwawa la kuhifadhi tope taka (Tailings) (Tailings Storage Facility -TSF). Baada ya kutembelea maeneo ya kituo tajwa hapo juu, Mwenyekiti wa Kamati aliongoza kikao cha majumuisho kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano kituoni hapo.
Wakati wa ziara na kiakao cha majumuisho wajumbe kwa ujumla waliipongeza Wizara ya Madini na STAMICO kwa ujenzi na usimamizi wa vituo hivyo. Aidha, walisisitiza Shirika kuendelea kukiimarisha. Sambamba na pongezi, wajumbe wa Kamati walikuwa na ushauri na maelekezo kwenye masuala mahsusi ya uendeshaji kama ifuatavyo:
i. Kituo kitekeleze majukumu yake bila kuchafua mazingira, hususan kwa kuhakikisha kuwa tope sumu toka kwenye TSF halisambai kwenye maeneo ya jirani. Pia kuwepo na utaratibu wa kuchukua na kuchunguza sampuli za maji na tope toka kwenye TSF kwa ajili ya kuangalia uwezekano na viwango vya uchafuzi (monitoring).
ii. Uwezo wa mtambo wa CIP ni mdogo kiasi cha kutotosheleza mahitaji ya wachimbaji kimamilifu. Mtambo huo unatakiwa ufanyiwe upanuzi sambamba na marekebisho kwenye sehemu ya kuingizia mbale (Ore feeding area) ikiwemo aidha kujenga ramp au kutumia hydraulic gun.
iii. Eneo la kituo linaonekana kuwa dogo hivyo kutotoa fursa kwa ajili ya upanuzi wa baadhi ya miundombinu kama TSF.
iv. Timu ya Usimamizi na uendeshaji kituo iongeze juhudi za kuwatafuta wateja ili kuongeza idadi ya wanaohudumiwa na mapato.
Kwenye majibu ya kuhitimisha Naibu Waziri alikubaliana na maelekezo yote ya Kamati; na kuahidi kuwa yatafanyiwa kazi kwa uzito na uharaka.