News
WAFANYAKAZI STAMICO WATAKIWA KUWA WABUNIFU NA KUACHA KUFANYA KAZI KWA MAZOEA
Wafanyakazi wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) wametakiwa kuwa wabunifu na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
Wito huo umetolewa leo tarehe 23 Februari, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt.Venance Mwasse wakati akifungua mkutano wa kila mwaka wa wafanyakazi wote wa Shirika kwenye Mgodi wa Kiwira,uliopo katika Wilaya ya Ileje, Mkoa wa Songwe.
Amesema kuwa ufanisi uwe ni msingi na dira ya kila mfanyakazi ili Shirika liboreshe utendaji wa shughuli zake na kupata faida.
"Katika safari hii ya mabadiliko ambayo tumeianza miaka minne iliyopita,najua kutakuwepo na nafasi ya kupambana na mawazo hasi.Hali hii ni ya kawaida katika maisha lakini tunatakiwa tuishinde kwa kuongeza bidii", alisema Dk Mwasse na kuongeza:
"Kama alivyosema Rais wetu Dk Samia Suluhu Hassan,nia nzuri huwa haishindwi.Naamini tutafikia malengo yetu ambayo ni kwa manufaa ya umma na sio ya mtu mmoja mmoja".
Amewataka wafanyakazi kuwa mabalozi wazuri kwa kuelezea wafanyakazi na wadau wengine kuhusu mafanikio na mageuzi yanayoendelea ndani ya Shirika.
"Wote tukitoka hapa tuwe na mtizamo chanya kuhusu Shirika letu na tutaendelea kutoa mafunzo ya kila mara ili kuwajengea wafanyakazi uwezo.
Wafanyakazi pia walipata nafasi ya kupata mafunzo kuhusu mtizamo wa kibiashara kutoka kwa Dkt Ernest Mwasalwiba,Mkufunzi katika Chuo Kikuu Mzumbe.
Aidha,wafanyakazi walipata nafasi ya kutembelea mtambo wa kisasa wa kusaga makaa ya mawe na kiwanda cha kuzalisha nishati safi na salama ya kupikia ya Rafiki Briquettes.
Mkutano huu umetanguliwa na kikao cha Baraza la Wafanyakazi kilichofanyika jana tarehe 22 Februari, 2025 na kufunguliwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini,Ndugu Msafiri Mbibo ambaye alilipongeza Shirika kwa mafanikio yaliyopatikana kwa kipindi cha muda mfupi na hasa kuanza kujitegemea kwa kugharamia shughuli zake kwa asilimia 100 ikiwa ni pamoja na kujilipa mishahara.