Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Madini la Taifa

STAMICO YAONGEZA KIWANDA KIKUBWA CHA KISASA CHA NISHATI SAFI YA KUPIKIA YA RAFIKI BRIQUETTES

Imewekwa: 09 November, 2026
STAMICO YAONGEZA KIWANDA KIKUBWA CHA KISASA CHA NISHATI SAFI YA KUPIKIA YA RAFIKI BRIQUETTES

SHIRIKA la Madini la Taifa (STAMICO) limezindua kiwanda kikubwa na cha kisasa cha kuzalisha nishati safi na salama ya kupikia ya Rafiki Briquettes jijini Dodoma, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa nishati hiyo, kukuza viwanda vya ndani na kuimarisha mchango wa sekta ya madini katika maendeleo ya taifa.

Uzinduzi wa kiwanda hicho uliofanyika Novemba 7, 2026, katika Kata ya Chigongwe, jijini Dodoma, umefanywa na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse, amesema kiwanda hicho ni cha nne cha Rafiki Briquettes kuzinduliwa nchini, kikiwa na uwezo wa kuzalisha tani 20 za nishati safi ya kupikia kwa saa.

Amesema kiwanda hicho kimegharimu Sh bilioni 3.70, huku uwekezaji wa jumla wa miundombinu na vifaa vilivyozinduliwa katika hafla hiyo ukifikia Sh bilioni 6.09, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa STAMICO wa kuongeza thamani ya rasilimali za madini na kuimarisha uzalishaji wa bidhaa zinazowanufaisha Watanzania.

Dkt. Mwasse amesema STAMICO imeendelea kutekeleza mageuzi kupitia mkakati wa MASTASHA (Make STAMICO Shine Again), unaolenga kuifanya kampuni hiyo kuwa miongoni mwa mashirika yenye ufanisi na uwezo wa ushindani katika sekta ya madini.

Amesema uwekezaji katika kiwanda hicho unaunga mkono dhamira ya Serikali ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, kwa kuwa Rafiki Briquettes inatoa fursa ya kupunguza matumizi ya kuni na mkaa na kuimarisha upatikanaji wa nishati mbadala inayozalishwa nchini.

Ameongeza kuwa moja ya manufaa makubwa ya uwekezaji huo ni kukuza viwanda vya ndani kupitia teknolojia ya uchakataji wa madini na matumizi ya rasilimali zilizopo nchini, huku ukifungua fursa za uwekezaji, biashara na ajira kwa Watanzania.

Katika kuimarisha upatikanaji wa bidhaa hiyo kwa wananchi, Dkt. Mwasse amesema STAMICO imezindua pia vifaa vya usambazaji ikiwemo pikipiki za magurudumu matatu maarufu kama Toyo, makontena 20 ya kuhifadhi na kusambazia nishati hiyo, mtambo mkubwa wa uchorongaji miti na malori mawili ya usafirishaji.

Amesema pikipiki hizo 30 zitagawiwa katika mikoa mbalimbali nchini kwa ajili ya kurahisisha usambazaji wa Rafiki Briquettes, huku makontena yakisambazwa Tanzania Bara na Visiwani ili kuongeza upatikanaji wa nishati hiyo katika maeneo mbalimbali.

Amefafanua kuwa vifaa hivyo vitasaidia kuwawezesha mawakala na wajasiriamali, wakiwemo wanawake na vijana, kushiriki katika biashara ya usambazaji wa nishati safi ya kupikia na hivyo kujipatia kipato.

Aidha, amesema STAMICO inaendelea kuimarisha shughuli zake za uchimbaji na biashara ya madini katika maeneo yake sita kwa kuongeza mitambo ya kisasa, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji, kukuza ajira na kuimarisha uwezo wa shirika kujitegemea kiuchumi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya STAMICO ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Simon Sirro, amesema uzinduzi wa kiwanda hicho ni matokeo ya mikakati na ushirikiano kati ya bodi na menejimenti ya shirika katika kuhakikisha STAMICO inaendelea kuimarika na kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Amesema bodi itaendelea kusimamia utekelezaji wa mikataba na mipango ya shirika ili kuhakikisha uwekezaji unaofanyika unaleta tija kwa taifa na kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Mhe. Sirro ametoa wito kwa wananchi wa Dodoma na Watanzania kwa ujumla kutumia nishati safi ya Rafiki Briquettes, akisisitiza kuwa ushiriki wa wananchi ni muhimu katika kufanikisha malengo ya Serikali ya kupunguza matumizi ya nishati chafu.

Aidha, ameiomba STAMICO kuimarisha mikakati ya kujitangaza na kupanua masoko ya bidhaa hiyo, huku akizitaka taasisi za umma, hususan shule na magereza, kuanza kutumia Rafiki Briquettes ili kuongeza mahitaji na kusaidia upanuzi wa uzalishaji.

Amesisitiza pia umuhimu wa wananchi na wadau wa nishati safi kuzingatia utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti na kutumia teknolojia zinazopunguza athari za kimazingira.

Uzinduzi wa kiwanda hicho ni sehemu ya juhudi za STAMICO za kuongeza thamani ya rasilimali za madini nchini, kukuza viwanda vya ndani na kuchangia utekelezaji wa dhamira ya taifa ya kuhakikisha nishati safi ya kupikia inapatikana kwa wananchi kwa gharama nafuu na kwa uhakika

 

Mrejesho, Malalamiko au Wazo

slot gacor